Mkurugenzi mpya wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) nchini Tanzania bwana Andrew Karas amefanya ziara ya kikazi katika ofisi ya makao makuu ya Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) na kulitaka Baraza hili kuhakikisha linapanua wigo wake kuwafikia watu wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini.






Katika Picha ya pamoja bwana Karas akiwa na wajumbe kutoka NACOPHA


Bwana Karas ametoa wito huo jijini Dar es salaam Septemba, 15, 2017, katika ziara yake ya kikazi iliyoambatana na kupata mrejesho wa utekelezaji wa mradi wa SAUTI YETU unaofadhiliwa na USAID kupitia Baraza tangu Decemba, 2013.
Aidha amesema kuwafikia watu wanaoishi na VVU na kuwapatia huduma nikumuenzi muasisi wataifa hili Mwalimu J.K Nyerere ambaye alikuwa muumini wa upendo, amani,umoja na mshikamano na kuongeza kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI yanahitaji mshikamano ili kufikia lengo la kuwa naTanzania isiyokuwa na maambukizo mapya.“Tusimuache mtu nyuma katika hali yoyote, tusonge mbele kwa pamoja huku tukidumisha amani, umoja na mshikamano."Alisema bwana Karas.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa Baraza bwana Deogratius P. Rutatwa amemshukuru bwana Karas kwa msaada wanaoutoa na juhudi zao katika mapambano dhidi ya UKIMWI hapa nchini na mataifa mengine kwa ujumla.
Amesema kwa sasa Baraza lipo katika wilaya 154 za Tanzania bara ambapo ni sawa na asilimia 82%, na zaidi ya watu laki sita wanaoishi na VVU wamefikiwa na Baraza. Kupitia mradi wa SAUTI YETU wilaya  29 tayari zimefikiwa ambapo mradi unatarajiwa kufikia wilaya 46.
Bwana Rutatwa ameongeza kuwa Baraza limefanikiwa kuongeza ushiriki wa WAVIU kuanzia ngazi ya jamii kupitia vikundi vya watu wanaishi na VVU. Vikundi vya WAVIU 3824 vimeundwa ili kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali za kiafya, kijamii na kiuchumi kuanzia ngazi ya jamii ili kufanikisha kufikia lengo la 90-90-90 ifikapo mwaka 2030. 
“Ushirikishwaji wa watu wanaoishi na VVU umehamasisha uwajibikaji, upatikanaji wahuduma za UKIMWI kutoka ngazi ya jamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI.”Ameeleza bwana Rutatwa.
Kuanzia mwaka 2016 Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) linaongoza kwa kutoa ufadhili wa shughuli za NACOPHA kwa asilimia 41.45% ikifuatiwa na mashirika mengine kama Global Fund asilimia 35.4% Umoja wa Mataifa (UN) 9.5% na Serikali ya Tanzania asilimia 6.1%.