NACOPHA KANDA YA MWANZA YAFANYA TATHMINI YA MRADI WA SAUTI YETU

NACOPHA Kanda ya Mwanza imefanya Mkutano  wa kutathmini mwenendo wa mradi wa SAUTI YETU unaotekelezwa na NACOPHA kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), katika Halmashauri nane za Mikoa ya Kanda ya Mwanza . Mkutano huu umefanyika tarehe 05/07/2018 Monarch hotel Jijini Mwanza.


Mkutano huo ulihudhuliwa na wenyeviti na Makatibu wa  Konga, pamoja na Waratibu wa Kuthibiti UKIMWI Halmashauri ( CHAC na DAC) kutoka katika wilaya za Nyamagana, Ilemela, Sengerema, Muleba, Musoma, Nzega Igunga na Kahama mji.


Mkutano huo ulifunguliwa na Mratibu wa UKIMWI mkoa wa Mwanza, lakini pia Ulihudhuriwa na Mratibu wa Kuthibiti UKIMWI TACAIDS Mkoa wa Mwanza, Mwenyekiti wa Baraza na baadhi  ya wajumbe wa Bodi, Afisa mtendaji mkuu na watendaji wa Baraza.


Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kutathmini mwenendo wa utekelezaji wa Mradi wa SAUTI YETU, mafanikio na Changamoto zinazopatikana katika kipindi cha utekelezaji cha mradi,  lakini pia kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto hizo kwa pamoja ili kufikia malengo yaliyoadhimiwa na Mradi wa SAUTI YETU.
UCHAGUZI WA KONGA WILAYA YA MULEBA DC

Konga ya Wilaya ya Muleba imefanya uchaguzi, wa kuwachagua viongozi wapya baada ya viongozi wa awali kumaliza muhula wao wa kwanza.

Uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba ambapo uliratibiwa na kusimamiwa na Afisa wa Asasi na uimarishaji ubora Bwana Joseph Bukula wa shirika la JSI R& T kupitia mradi wa CHSSP Unaofadhiliwa na shirika la msaada kutoka kwa watu wa Marekani USAID, NACOPHA Kanda ya Mwanza na Ofisi ya maendeleo ya jamii chini ya Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Halmashauri ya  Wilaya ya Muleba

Uchaguzi huo ulihudhuliwa wa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la watu wanaoshi na VVU bwana Deogratius Rutatwa, Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii, Mratibu wa UKIMWI wilaya upande wa tiba (DACC), Mratibu wa UKIMWI wilaya upande wa jamii (CHAC), Mratibu wa Kanda – NACOPHA/SAUTI YETU, Afisa tathmini na ufuatiliaji – NACOPHA/SAUTI YETU, Afisa wa asasi na uimarishaji ubora – JSI R&T/CHSSP, na wajumbe kutoka viikundi 25 vya WAVIU wilaya ya Muleba.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na:
Romward Nkororo – Mwenyekiti wa Konga
Malapia Athanasio – Makamu Mwenyekiti
Lameki Ndyamukama – Katibu wa Konga
Febronia Paskali – Mhasibu wa Konga

Viongozi wengine waliochaguliwa ni wajumbe wanne wa Konga, Uwakilishi wa Vijana pamoja na wajumbe wawili watakao wakilisha katika kamati ya kudhibiti UKIMWI ya Wilaya (CMAC)
Baraza kupitia Afisa Mtendaji Mkuu inatoa pongezi kwa viongozi waliochaguliwa na kuwataka watekeleze wajibu wao kufuatana na sheria ya baraza inavyowataka wafanye. Hivi sasa Baraza lina konga zipatazo 154. 

Baraza linatoa shukrani za dhati kwa JSI R&T kupitia mradi wa CHSSP kwa kufanya kazi kwa Karibu na Baraza kwa kuhakikisha malengo ya pamoja ya kufikia 90-90-90 yanafikiwa.


TANZIA: MAKAMU MWENYEKITI WA BARAZA LA TAIFA LA WATU WANAOISHI NA VVU TANZANIA (NACOPHA) Bi.THEREZA MICHAEL AFARIKI DUNIA.

BARAZA LA TAIFA LA WATU WANAOISHI NA VVU TANZANIA (NACOPHA ) Limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Makamu Mwenyekiti wa Baraza Bi.Thereza Michael kilichotokea leo mchana katika hospitali ya mkoa alipolazwa kwa matibabu Mjini Musoma. 
Uongozi wa NACOPHA unatoa pole na kuungana na Familia ya Marehemu, Ndugu , Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huu, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Pumzika kwa Amani Ndugu yetu Mpendwa

TACAIDS KUANZA KAMPENI YA KUHAMASISHA WANAUME KUPIMA AFYA ZAO-MABOKO

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
TUME ya Taifa ya kudhibiti ukimwi (TACAIDS), inatarajia kuanza kampeni za kitaifa kuhamasisha wanaume kupima afya zao ,ili kujenga tabia ya kujitokeza kujua afya zao kwani ni asilimia 45 pekee ya kundi hilo walioaminika kuwa na VVU ndio waliopima kujua hali zao.
Aidha imeeleza ,kati ya watu kumi wenye maambukizi mapya kwa mwaka ,vijana wanne sawa na asilimia 40 ugundulika kupata maambukizi hayo.
Pamoja na hayo ,kati ya vijana kumi waliopata maambukizi mapya kila mwaka nane huwa vijana wa kike na wawili ni vijana wa kiume.IMG_9486
Mratibu wa mtandao wa viongozi wa dini wanaoishi na virusi vya ukimwi ,(TANERELA),mchungaji Amin Sandewa pichani .(picha na Mwamvua Mwinyi)
IMG_20180301_160202
Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti ukimwi (TACAIDS ) ,Leonard Maboko akizungumza jambo ,mjini Kibaha ,Mkoani Pwani ,katika mkutano ulioandaliwa na tume hiyo ,kupitia mipango ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli ya mwaka 2018/2019 .(picha na Mwamvua Mwinyi)
………………………………………………………………………

Mkurugenzi mtendaji wa TACAIDS ,Leonard Maboko aliyaeleza hayo mjini Kibaha ,Mkoani Pwani ,katika mkutano ulioandaliwa na tume hiyo ,kupitia mipango ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli ya mwaka 2018/2019 .
Alisema ,kampeni hiyo itakuwa ya miezi sita na itakuwa endelevu hadi hapo watakapohakikisha wanatokomeza ama kupunguza gonjwa hilo .
Maboko alisema  ,wale watakaobainika kuwa na maambukizi mapya watatakiwa kuanza tiba ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) mapema ili kuondoa vifo vinavyotokana na virusi hivyo .
Alielezea ,wanaandaa kampeni hizo kutokana na takwimu za utafiti wa viashiria vya ukimwi ya mwaka 2016/2017 inayoonyesha idadi ya watu wanaopima na wanaogundulika kuambukizwa wanaoanza kutumia dawa ni wanawake kuliko wanaume.
“Asilimia 45 ya wanaume ndio wanaoaminika kuwa wamepima na kujua hali zao ,hali ambayo inaonyesha ni kiwango cha chini “.
“Simaanishi wenye ukimwi wote wameshapima kujitambua ,lakini inahitajika hamasa ili tufikie malengo”alisema Maboko.
Hata hivyo Maboko alisema ,maambukizi mapya ya ukimwi yanaongezeka zaidi kwa kundi la vijana hususan wa kike .
“Hii inaonyesha huko kipindi cha nyuma hakukuwa na hali hiyo hivyo haina budi kundi hilo likatiliwa mkazo ,ili kupunguza ongezeko hilo ” 
“Hali ya maambukizi ya ukimwi Tanzania kwasasa ni asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.1 ,hali inapungua lakini inatakiwa tuendelee kupambana na maambukizi mapya ,na Tanzania bila ukimwi inawezekana” alisema Maboko.
Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo ,kuwa asasi mwamvuli zinarahisisha kazi ya uratibu kwa TACAIDS lakini changamoto waliyonayo ni kutopata ripoti za asasi hizo .
Nae mratibu wa mtandao wa viongozi wa dini wanaoishi na virusi vya ukimwi ,(TANERELA),mchungaji Amin Sandewa alisema wanawajengea uwezo wa kielimu viongozi wa dini wanaoishi na virusi hivyo ili kupambana na ukimwi na kuwa vielelezo kwa wengine.
Sandewa alisema, ugonjwa huo hauchagui ,muumini,viongozi wa dini wala mwalimu hivyo aliiomba jamii kuachana na unyanyapaa.
Meneja ufuatiliaji na takwimu ,kutoka baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (NACOPHA) ,Rachel Jacob alifafanua wanaratibu shughuli za masuala ya ukimwi kwa kulenga mtu mmoja mmoja,kundi na mtandao .
Kwa mujibu wake ,katika kufanikisha shughuli hizo wameshafikia halmashauri 154 nchini kwa kushirikiana na viongozi walioteuliwa ambao wana maambukizi kwa ajili ya kusaidia kuwafikia watu na vikundi hivyo .
Rachel alibainisha ,kwasasa wana wajumbe 616,984 miongoni mwao asilimia 44 ni wanaume waliojitokeza kuweka wazi afya zao .
Alifafanua zoezi hilo nao wanaendelea nalo ,kuhakikisha kufikia halmashauri zote hasa kundi la wanaume ambalo bado halina mwamko huo.
Katika mkutano huo ,asasi mwamvuli zilizoshiriki ni pamoja na NACOPHA,TAIFO,BAKWATA,
FAJISAM-PENTECOSTE,TANERELA,TEC,BAHAI,National Steering Committe, na TIENAI.

AGPAHI YAENDESHA WARSHA KWA WAVIU WASHAURI HALMASHAURI SITA ZA WILAYA MKOA WA SHINYANGA

Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha    na mapambano dhidi ya 

Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limeendesha warsha kwa WAVIU Washauri 75 kutoka halmashauri sita za wilaya mkoa wa Shinyanga ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).
WAVIU washauri ni watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na wamejiweka wazi na huru kuwashauri watu wanaoishi na VVU katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa,kutoa ushauri nasaha kwa wenzao,kujitolea kufuatilia na kufundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha sambamba na kuhamasisha WAVIU wenzao kujiunga katika vikundi ili kusaidiana na kupunguza unyanyapaa.
Warsha hiyo ya siku tatu imeanza Jumatatu Januari 29,2018 katika ukumbi wa Karena Hotel Mjini Shinyanga na kukutanisha pamoja WAVIU Washauri takribani 75 kutoka halmashauri za wilaya za Kishapu, Manispaa ya Shinyanga, Shinyanga, Kahama Mji, Ushetu na Msalala.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mratibu wa Masuala ya Watoto,Mama na Baba kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Aminael Tesha alisema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo WAVIU Washauri ili waweze kuwaunganisha wateja kutoka kwenye jamii kwenda kwenye vituo vya tiba na matunzo na kuwafuatilia wateja waliopotea katika huduma na kuwarudisha kwenye huduma.
“Kupitia warsha hii tutapeana mikakati mbalimbali jinsi ya kuwatafuta wateja waliopotea katika huduma na kujadili namna ya kuboresha zaidi huduma katika vituo vya tiba na matunzo lakini pia kutoa elimu kuhusu haki za WAVIU Washauri”,alieleza Tesha.
Naye Mratibu wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), kanda ya Mwanza, Veronica Joseph aliwasihi watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kujiweka wazi kwani itawasaidia kupata msaada kwa watu wanaowazunguka ikiwemo familia zao.
“Wale ambao hamjapima nawashauri mpime ili mjue afya zenu na ukibainika una maambukizi ya VVU jiweke wazi ili usaidiwe,kujiweka wazi kutakusaidia kuondoa matatizo na utaweza kupata fursa mbalimbali kutoka wafadhili”,alileleza.
Katika hatua nyingine alisema shirika la AGPAHI linatekeleza miradi ya Ukimwi katika mikoa sita nchini ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita,Mwanza, Tanga na Mara kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control and Preventation (CDC).

Mratibu wa Masuala ya Watoto,Mama na Baba kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Aminael Tesha akizungumza wakati wa warsha ya siku tatu ya WAVIU Washauri halmashauri sita za wilaya mkoa wa Shinyanga iliyofanyika katika ukumbi wa Karena Hotel Mjini Shinyanga.

Aminael Tesha akielezea malengo ya warsha hiyo.

Mwezeshaji katika warsha hiyo, Veronica Joseph ambaye ni Mratibu wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), kanda ya Ziwa, akielezea kuhusu umuhimu wa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kufubaza makali ya VVU na kujiweka wazi.

MVIU Mshauri, Joyce Philimon kutoka mkoani Simiyu ambaye anaishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 1997 akielezea umuhimu wa kujiweka wazi pale unapobaini kuwa umepata maambukizi ya VVU. Kujiweka wazi kwa Joyce kumfanya aishi salama na kwa amani na kupata fursa za kushiriki shughuli mbalimbali kutoka kwa wadau.  


MVIU Mshauri Seleman Habibu kutoka Kahama akielezea namna alivyoweza kuishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 2000 na ana watoto wawili ambao hawana maambukizi ya VVU na mke wake pia hana maambukizi ya VVU.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU katika Manispaa ya Shinyanga,Vedastus Mutangira akizungumza katika warsha hiyo ambapo akiwasisitiza watu wanaoishi na VVU kumeza dawa kwa utaratibu sahihi uliowekwa pamoja na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.

WAVIU Washauri wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yanajiri ukumbini.

Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini.

Mwezeshaji katika warsha hiyo,Vedastus Mutangira akitoa elimu kuhusu VVU na Ukimwi. Aliwasisitiza watu wanaoishi na VVU kumeza dawa kwa utaratibu sahihi uliowekwa pamoja na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.

MVIU Mshauri Neema Anthony kutoka kutoka CTC ya Segese katika halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.