Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (#NACOPHA) Kupitia ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa la kupambana na UKIMWI (#UNAIDS) liliandaa ziara ya siku mbili ya kuongeza ujuzi kwa konga zake na halmashauri katika kuongeza hamasa ya upimaji na ufuasi wa dawa kwa kupitia mbinu ya kushirikishana uzoefu baina ya konga zake katika masuala mazima ya Usimamizi, uendeshaji, ustawi pamoja na faida ya uwepo wa vikundi wezeshi kwa Watu wanaoishi na VVU pamoja na Halmashauri kwa ujumla.


kutokana na hatua kubwa ambayo halmashauri ya Mbozi imepiga katika shughuli zake za muitikio wa UKIMWI kupitia ushirikishwaji wa konga pamoja na usimamizi mzuri wa vikundi vya wezeshi vya watu wanaoishi na VVU (Vikundi Wezeshi) Baraza lilichagua halmashauri hiyo kuwa wenyeji wa ziara hiyo ya siku mbili kwa wajumbe kutokea katika halmashauri nne za Songea Dc, Makete, Njombe Dc pamoja na Rungwe Dc kusafiri na kwenda kujifunza na kubadilishana uzoefu na halmashauri ya Mbozi katika masula mazima ya uhamasishaji upimaji na ufuasi mzuri wa dawa kupitia vikundi wezeshi vya WAVIU.

 
 Ziara hii ilijumuhisha viongozi wa konga, wenyeviti wa kamati ya kudhibiti UKIMWI (CMACs), waratibu wa UKIMWI ngazi ya halmashauri (CHACs), wawakilishi wa viongozi wa vikundi vya WAVIU kutokea katika halmashauri tajwa. Ziara hii ilikuwa yenye mafanikio makubwa kwani kupitia wenyeji ambao ni Mbozi waliweza kushirikisha konga alikwa zote na kujionea namna gani konga ya Mbozi imepiga hatua kubwa katika muitikio wa UKIMWI, maendeleo ya vikundi wezeshi pamoja na ufuasi mzuri wa dawa kwa WAVIU ndani ya halmashauri.


Wajumbe waliweza kutembelea mojawapo ya kituo cha tiba na matunzo (CTC) na kujifunza namna ya ushirikishwaji wa WAVIU kama watoa huduma ndani ya jamii ulivyoweza kupunguza changamoto ya utoro wa dawa na kuongeza hamasa ya upimaji kwa jamii, pia wajumbe waliweza kutembelea mojawapo ya kikundi wezeshi cha WAVIU kata ya ICHESA na kujionea namna ya mfano wa vikundi wezeshi unavyofanya kazi na kuleta mabadiliko chanya kwa WAVIU na halmashauri kwa ujumla. 


Mwisho wa ziara wajumbe wote kutokea halmashauri zote nne waliweza kutoa ushuhuda wao wa namna gani wamefurahia na kujifunza kupitia ziara hii kisha kuhaidi kwenda kufanyia kazi maeneo ambayo walibaini ni mapungufu yao ambayo yanasababisha kwa namna moja ama nyingine kutofika kiwango cha maendeleo kama halmashauri ya Mbozi walichokifikia na watafanya hivyo baada ya kurejea katika halmashauri zao.



Wenyeviti wa halmashauri pamoja na mkurugenzi wa halmashauri ya Mbozi walitoa shukrani zao kwa UNAIDS kupitia NACOPHA kwa kuwezesha ziara hii na kuomba pale inapowezekana kuendelea kuwezesha halmashauri zingine kuja kutembelea na kujifunza katika halmashauri ya Mbozi.