Shirika la afya duniani WHO limetoa miongozo mipya kuhusiana na upimaji wa virusi vya HIV kutekelezwa na watu binafsi ili kuboresha huduma ya upimaji wa virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi.

Lesotho Mobile Gesundheitsversorgung: Bluttests (picture-alliance/AP Photo/D. Farrell)
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la afya duniani WHO, kuhusu hatua zilizopigwa kupambana na ukimwi duniani, ukosefu wa upimaji wa virusi vya HIV vijulikanavyo kama VVU ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa mapendekezo ya shirika hilo yanayotaka kila mwenye virusi vya VVU apatiwe dawa za ART za kukata makali ya ugonjwa wa Ukimwi.
Ripoti hiyo imegundua kuwa zaidi ya watu milioni 18 wenye virusi vya HIV duniani wanatumia dawa hizo za kukata makali ya Ukimwi  na idadi sawa na hiyo bado hawajaweza kupata matibabu, kutokana na kutojua hali zao.
Hivi sasa asilimia 40 ambayo ni zaidi ya watu milioni 14 duniani wanaoishi na virusi vya HIV hawajui hali yao ya HIV.Wengi wa watu hao wako katika hatari zaidi ya kuambukiza HIV na mara nyingi hupata ugumu wa kufikia huduma za afya za kupimwa .
Asilimia 40 ya wanaoishi na HIV hawajui
Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan amesema mamilioni ya watu walio na HIV bado hawapokei matibabu ya kuyaokoa maisha yao ambayo pia yanaweza kuepeusha maambukizi kwa wengine.
HIV self testing (Imperial College London/T. Angus)
Kifaa cha kujipima mwenyewe HIV
Chan amesema kujipima virusi hivyo kutafungua milango kwa watu wengine kujua hali zao na kutafuta jinsi ya kupata matibabu na huduma za kuzuia maambukizi.Mkurugenzi wa idara ya HIV na ukimwi wa WHO Dr Gottfried Hirnschall anahimiza watu kujua hali zao mara kwa mara.
Kujipima virusi vya Ukimwi kunamaanisha kuwa watu wanaweza kutumia mate au damu ya kidoleni kujua hali zao na matokeo yanakuwa tayari ndani ya dakika 20 au hata muda chache zaidi ya hapo.
Wale wanaojipata wana virusi vya HIV wanashauriwa kwenda katika vituo vya afya ili kuthibitisha matokeo hayo. WHO inapendekeza wapewe taarifa na ushauri nasaha pamoja na matibabu ya haraka.
Kujipima mwenyewe HIV kunanuia kuwafikia watu wengi zaidi ambao bado hawajajua hali zao, kuwashajaisha watu, kugundua mapema kabla ya hali zao za afya kuwa mbaya, kuleta huduma karibu na wanapoishi na kuongeza hamu ya watu kutaka kujua hali zao.
Wanawake wengi  wanajua hali zao kuliko wanaume
Utafiti unaonyesha kuwa wanawake wengi hujitokeza kutaka kujua hali zao za Ukimwi na kupokea matibabu punde wanapojua wameathirika ikilinganishwa na wanaume. Ni asilimia 30 tu ya wanaume duniani ambao wamepimwa HIV.
Lesotho Mobile Gesundheitsversorgung: Bluttests (picture-alliance/dpa/D. Kurokawa)
Kituo cha kupima Ukimwi Lesotho
Hiyo inamaanisha kuwa ni vigumu kujua ni wanaume gani katika jamii wameathirika, kuwaweka katika matibabu na huenda wakafariki mapema zaidi kutokana na magonjwa nyemelevu yanayosababishwa na ukosefu wa kinga mwilini au Ukimwi kuliko wanawake.
Wasichana wadogo na wanawake mashariki na kusini mwa Afrika pia inaripotiwa kuwa wanakumba na  hatari kubwa ya maambukizi mara nane kuliko wenzao wa kiume. Ni chini ya msichana mmoja aliye kati ya umri wa miaka 15 hadi 19 anayejua hali yake ya HIV katika kanda hizo za Afrika.
Mashoga, watumiaji wa dawa za kulevya na wafungwa magerezani pia hawapimwi kujua hali zao. Makundi haya ya watu yanawakilisha asilimia 44 ya watu milioni 1.9 duniani walio na maambukizi mapya ya HIV kila mwaka.
Mwandishi: Caro Robi
Mhariri: Tatu Karema