BARAZA la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) linaungana na Watanzania pamoja na wadau wote katika maadhimisho ya siku ya watu wenye Ualbino yenye kauli mbiu “HAKI YA UJUMUISHI HAKI YA USHIRIKI, WATOTO WENYE UALBINO WASIKILIZWE, WALINDWE”


Katika kuadhimisha siku hii muhimu NACOPHA inawahamasisha watu wote wenye Ualbino na wasiokuwa na Ualbino kupima Afya ili kujua hali zao za maambukizi ili kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza ongezeko la maambukizi ya Virusi vya UKIMWI mpaka asilimia 90 ifikapo 2030.  Kujua hali ya maambukizi kunamsaidia mtu kuanza Tiba mapema endapo tu atagundulika kuwa ana Virusi vya UKIMWI.

Aidha NACOPHA inatoa wito kwa jamii kuwalinda watu wenye Ualbino kwa kuondokana na dhana potofu ya kuwauwa, kuwasababishia ulemavu.
 Pia kuondokana na imani potofu kuwa mtu mwenye VVU anaweza kupona kwa kufanya ngono na mtu mwenye Ualbino, ni vyema ikafahamika kuwa bado hakuna dawa ya kuponyesha ama kuondoa kabisa Virusi vya UKIMWI.

Dhana hiyo ni potofu na huchangia ongezeko la maambukizi kwa watu wenye Ualbino. Sisi sote ni binadamu, hivyo hatuna budi kupendana, kulindana na kutobaguana.


NACOPHA inawakumbusha Watu wote wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kuendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV), kubaki kwenye tiba ili kuweza kupunguza wingi wa VVU kwenye damu zao.