Kila ifikapo tarehe 16 June kila mwaka nchi za Bara la Afrika zinaazimisha siku ya mtoto wa Afrika ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwakumbuka watoto waliokufa huko Soweto nchini Afrika ya Kusini mwaka 1976.
Serikali, Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa pamoja na wadau mbalimbali kwa pamoja hutumia siku hii kujadili changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, kutokuwa na sheria za kuwalinda watoto katika changamoto hizi.
Kwa mujibu wa ripoti dhidi ya ukatili wa watoto Tanzania (RUDWT) iliotolewa mwaka 2009 ilisema takribani Wasichana 3   kati ya 10  na Mvulana 1 kati ya 7 walifanyiwa ukatili wa kijinsia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, huku karibia 6% ya wasichana walilazimishwa kufanya ngono na wanaume waliowazidi umri  kabla ya kufikia umri wa miaka 18.
Ni wazi kuwa watoto wengi hususani wakike wamekuwa wakilazimishwa kufanya ngono na watu waliowazidi umri ambapo wengi wao huambukizwa Virusi Vya UKIMWI na magonjwa mengine ya Ngono, lakini wengi wao huogopa kuwataja ama kusema wamefanyiwa ukatili huo kutokana na wanaowafanyia kuwa ndugu wa karibu  sana pia huwatishia  kama watasema 
Changamoto kubwa iliopo ni kutokuwa na uwazi baina ya wazazi na watoto, pia kutokuwa na vyombo vinavyowalinda watoto wanaofanyiwa ukatili wa kingono.
Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU linaungana na wadau wote katika kuazimisha siku hii muhimu ya Mtoto wa Afrika, wito wetu kwa Serikali, Wadau mbalimbali wanaohusika na Watoto, mashirika ya dini, vyombo vya sheria na jamii kwa ujumla kuungana kwa pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya ukatili unaoweza kuwapelekea kupata maambukizo ya Virusi Vya UKIMWI na magonjwa mengine ya Ngono.  
Last Mlaki