WATU watakaogundulika kuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wataanza kupewa na kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa (ARVs) bila kusubiri kinga zao za mwili kupungua kama ilivyozoeleka.

Wakati utaratibu huo mpya ukitarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu, kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kupitia kwa Mwenyekiti wake, Constantine Kanyasu, imeshauri serikali kuangalia namna ya kuruhusu dawa ziingizwe na kuuzwa madukani kwa bei nafuu kwa ajili ya watu ambao hawako chini ya mpango wa serikali.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa kwenye kikao cha kamati hiyo ya Bunge ambayo ilipokea taarifa iliyofikiwa katika utafiti wa upatikanaji wa chanjo ya Ukimwi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulusubisya aliieleza kamati juu ya mabadiliko katika tiba na kusema mtu yeyote anayepima na kugundulika kuwa ana Virusi Vya Ukimwi, ataanza kupatiwa ARVs mara moja

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Dk Angela Ramadhani, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) yaliyotolewa mwaka jana baada ya tafiti kubainisha kuwa zipo faida za kuwahi kupata dawa husika.
Dk Ramadhani alisema maagizo hayo ya WHO yanatokana na tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali na kubainisha kuwa kutumia ARVs kabla ya kinga ya mwili kushuka, kuna faida kutokana na kuonesha kuwa kunakuwa na usalama zaidi.

Kwa mujibu wa Dk Ramadhani, baada ya mwongozo kutolewa mwaka jana, Aprili mwaka huu, shirika hilo liliita nchi wanachama na kusambaza taarifa hizo kwa ajili ya kuziwezesha kujipanga kiutekelezaji.
“WHO wakishatoa mwongozo, huita wataalamu na kuwaeleza ili nchi zijiendae. Kwa mfano, kama zina uwezo wa kutoa dawa hizo,” alisema Dk Ramadhani na kusema pia hapa nchini, wameanza wiki hii kupitia miongozo ya zamani kabla ya utaratibu huo mpya kuanza Oktoba mwaka huu.

Wakati huo huo, wakati wa kikao na Kamati ya Bunge baada ya wizara kuonesha kuwa uwezo wa serikali wa kutoa dawa hizo unaishia kwa watu milioni 1.3 licha ya kuwa na watu 2.4 wenye VVU, Mwenyekiti wa Kamati, Kanyasu alishauri suala hilo liangaliwe kwa umakini.

“Kama uwezo wa serikali unaishia kwa watu milioni 1.3, ni kwa nini serikali isijikite hawa wanaopata free (bure) halafu hawa private (binafsi) wakaruhusiwa kuingiza dawa zikauzwa kwenye maduka kwa bei nafuu ili mtu akishajiona ana Ukimwi aende akanunue ili kuziba pengo hilo la watu milioni 2.4,” alihoji Kanyasu wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Katika kikao hicho cha kamati na watendaji kutoka wizara, taarifa zilibainishwa kwamba wafadhili wamepunguza na wanaendelea kupunguza bajeti katika masuala ya Ukimwi.
Kuhusu chanjo, ilielezwa na Katibu Mkuu kwamba, shughuli zote zilizopangwa awali kuhusu chanjo zilisitishwa Juni, 2015 baada ya fedha kutoka kwa wafadhili kwisha jambo ambalo serikali imechagizwa kutoa fedha uendelee.

Ilisisitizwa kwamba Tanzania inapaswa ijikite kwenye chanjo ikizingatiwa kwamba haiwezi kutegemea tafiti za mataifa mengine kutokana na wadudu kutofautiana.

Wakati huo huo, kamati ilielezwa changamoto zilizopo kwenye utafiti juu ya suala la Ukimwi kwamba Watanzania wengi wanaogopa kuwekewa vimelea vya kupambana na Ukimwi wakidhani wakipandikiziwa watakuwa wameambukizwa. Katibu Mkuu alisema hali hiyo inasababisha watafiti kupata shida ya kupata watu wa kufanyia utafiti.

Awali, katika taarifa yake kuhusu utafiti wa chanjo ya Ukimwi, Katibu Mkuu alisema wizara yake kupitia Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mbeya zilifanya utafiti mwaka 2014.

Alisema kati ya Februari 2007 na Februari 2008, watu 162 miongoni mwa 177 walifanyiwa uchunguzi na chanjo kuonesha usalama mzuri na hakukuwa na madhara makubwa yanayohusiana moja kwa moja na chanjo.

Aidha, asilimia 100 ya washiriki waliopata chanjo halisi waliweza kutengeneza kinga zinazohusisha seli za kinga ya mwili na protini zilizoko kwenye damu dhidi ya VVU. Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza, mradi wa awamu ya pili ulifanyika Tanzania na Msumbiji

Source Habari Leo