BAADHI ya Wabunge wamependekeza Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008 kufanyiwa marekebisho ili kuwapima Watanzania wote Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa lazima hususan Wanaume badala ya kuwapima wanawake pekeyao wanapokwenda clinik
Kadhalika, wabunge wameahidi kuibana serikali iongeze fedha kwa ajili ya mapambano ya Ukimwi ili kunusuru maisha ya wanaoishi na VVU.
Wabunge hao ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, walitoa maoni hayo juzi jioni mjini Dodoma walipokutana na uongozi wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU (Nacopha).
Mkutano huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Msekwa, ulivuta hisia za wabunge hao na kujikuta wakiahidi kuibana serikali iongeze fedha katika bajeti ya mwaka 2018/2019.


Mbunge wa Nsimbo (CCM), Richard Mbogo, akizungumza katika mkutano huo alisema suala la kupima liwe la lazima na kwamba ana wasiwasi hilo likipitishwa wabunge wengi watakimbia kupima.
Alisema tatizo la Ukimwi linazidi kuwa kubwa na kwamba kuna haja serikali kuwasaidia Nacopha ili wafanye kazi yao vizuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Husna Mwilima, alisema itahakikisha bajeti ya mwaka 2018/2019 inatengewa fedha za kutosha kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi.
Katika kukabiliana na janga hilo, Mwilima aliwaambia wajumbe kuwa atahakikisha anashirikiana na wadau mbalimbali ili kuzindua kampeni maalum ya nchi nzima ya kumuwezesha kila mwanamke kutembea na kondomu katika mkoba wake kila anapokwenda.
Alisema kwa sasa hali ni mbaya hususan kwa wasichana wanaosoma vyuo vikuu na kwamba kuna taarifa msichana mmoja anakuwa na mahusiano na wanaume sita kwa wakati mmoja.
"Lazima hii kampeni iende nchi nzima kila mwanamke akitongozwa, ajue kondomu ni sehemu ya maisha yake kwa ajili ya kumlinda," alisema Kuhusu upimaji wa VVU, alisema lazima wabunge wote wapime japokuwa anajua wengi wao watakimbia.

Aliahidi kuunda kikosikazi ambacho kitashirikiana na Nacopha ili kuiambia serikali umuhimu wa kutenga fedha za kutosha kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi.
Akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kamati hiyo, Ofisa Mtendaji wa Nacopha, Deogratias Rutatwa, alisema mpaka sasa hakuna taasisi ya serikali inayotambua masuala ya watu waishio na VVU.
Rutatwa alisema licha ya Sheria ya Ukimwi kupitishwa na Bunge, lakini mpaka sasa haijaanza kutumika kwa madai kwamba miongozo yake haijawa tayari na kwamba serikali imeshindwa kuwafikia wanaoishi na VVU ili kujua matatizo yao.
Aliiomba kamati hiyo kuwasemea bungeni ili kuzishinikiza halmshauri mbalimbali nchini zishiriki moja kwa moja katika mapambano ya Ukimwi kuliko kazi hiyo kuachiwa mashirika binafsi.

Rutatwa alisema kwa sasa hali ni mbaya kwa kuwa serikali haitoi fedha huku wafadhili nao wakisitisha misaada.
Aidha, alisema kama wanaoishi na VVU wote nchini wakipewa dawa za kupunguza makali, zitawatosha kwa miezi mitano tu.
Alisema mwaka huu wa fedha zimetengwa fedha kidogo na kwamba kama hatua nyingine hazitachukuliwa, Watanzania wengi watakufa kwa kukosa dawa za ARVs.
Nacopha inafanya kazi katika wilaya zote hapa nchini chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).