MIKOA ya Njombe, Iringa na Mbeya yakabiliwa na maambukizi makubwa ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kutokana na muingiliano mkubwa wa watu unaosababishwa na shughuri za kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Tume ya kudhibiti Ukimwi (Tacaids) Mkoa wa Mbeya, Edwin Mweleka, wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye utambulisho wa mradi wa ushirikishaji wa wananchi wanaoishi na virusi vya Ukimwi wa ‘Sauti yetu’ unaofadhiliwa na wananchi wa Marekani kuipitia Shirika la USAID.
“Tunashukuru wenzetu wa Marekani kwa kutusaidia kufadhili mradi huu wa Sauti yetu kupitia shirika la USAID, na naamini kwa mikoa yetu hii yenye maambukizi makubwa, mradi huu utakuwa msaada mkubwa katika kupunguza maambukizi,” alisema.

Mweleka alisema kuwa mikoa ya Mbeya na Iringa haijawahi kutoka kwenye orodha ya mikoa mitatu yenye maambukizi makubwa tangu tafiti zilipoanza kufanyika katika miaka ya 2003/2004.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini, Justine Mwinuka, alisema mradi huo unatekelezwa katika halmashauri 46 zilizopewa kipaumbele nchi nzima huku katika Mkoa wa Mbeya zikihusika halmashauri tatu ambazo ni Mbeya jiji, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Alisema kuwa mradi huu unatambulishwa kwa waratibu wa Ukimwi shughuli za Ukimwi ngazi ya halmashauri pamoja na watendaji wa mabaraza ya watu wanaoishi na VVU ngazi za wilaya (Konga)
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo wa ‘Sauti Yetu’, Rachel Jacob, alisema changamoto inayowakumba watu wanaoishi na VVU kwa sasa ni unyanyapaa binafsi hali ambayo huwafanya watu hao kuishi kwa wasiwasi wakati wote
Alisema lengo kubwa la mradi huo ni kutoa hamasa kwa jamii kupima afya zao kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa ili kila mtu aweze kuijua afya yake na wale wanaokutwa na maambukizi waweze kuanzishiwa dawa.
Jacob alisema kuwa Mradi huo ulianza kutekelezwa tangu mwezi Oktoba 2015 na utakamilika mwezi Oktoba mwaka 2019.
Post a Comment