Suzan Athan James ni msichana wa miaka 21 anaeishi na Virusi vya UKIMWI, Suzan  aliezaliwa na maambukizo kutoka kwa wazazi wake waliokuwa wanaishi  mkoa wa Pwani katika  wilaya ya Bagamoyo.

Mama yake alifariki akiwa na umri wa miaka mitatu alibaki na baba yake lakini baada ya muda mfupi baba yake aliondoka na kuacha kumsaidia ndipo alipochukuliwa na bibi yake anaeishi nae mpaka sasa. Kutokana na ugumu wa maisha na kukosa Ada Suzan aliacha shule, na kuamua kwenda kujifunza ushonaji wa nguo kwa mtu binafsi, lakini malengo yake ni kumiliki biashara kubwa ya ushonaji wa nguo
Kutokana na umahiri wake wa kujituma na kujishughulisha Suzan alipata mfadhili ambae ni MR Chavanga kutoka kampuni ya Blue Sky films ya Nairob Kenya, aliejitolea kumzawadia Cherehani ili kurahisisha zaidi ndoto yake ya kujiajiri na  kumili biashara ya ushonaji wa nguo
Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) lilichukua jukumu la kufuatilia ahadi hiyo  na kuhakikisha inapatikana na hatimaye kuikabidhi kwa Zuzani mbele ya Afisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Bagamoyo Bi. Halima Shabani na mwenyekiti wa Konga ya Halmashauri ya Bagamoyo Bwana Saidi Alfan siku ya tarehe 6 Mei 2016.

Kwa upande wake Suzani alieonekana mwenye Furaha na Tabasamu wakati akikabidhiwa Zawadi hiyo na mwakilishi kutoka NACOPHA Afisa Mratibu wa Kanda Bwana Ally Mamlo, alishukuru na kuahidi kukitunza cherehani hicho “napenda kumshukuru sana mfadhili aliejitolea kunisaidia hiki cherehani, pia nawashukuru sana NACOPHA kwa kukifuatilia na kukileta hadi huku bagamoyo kwa kweli nimefurahi sana na nitakitumia kutimiza ndoto zangu Mungu awabariki sana”

Kwa upande wake afisa maendeleo ya ya jamii wa wilaya ya Bagamoyo Bi. Halima Shabani Simbano alilipongeza Baraza kwa kuwajali watu wanaoishi na VVU na kuwasihi kutoishia kwa Suzani bali waendelee kuwasaidia wengine wengi zaidi.

Mwenyekiti wa Konga katika Wilaya ya bagamoyo Bwana Saidi Alfan pamoja na kulishukuru Baraza kwa kazi nzuri linalofanya ya kuwajali WAVIU pia alimsihi Suzan kukitumia cherehani hicho vizuri na kukitunza, pia alimshauri kuwahamasisha vijana wengine wanaoishi na VVU kutojificha bali wajitokeze na kujiweka wazi hali zao za maambukizi kwani ndipo watakapo pata msaada wa aina mbalimbali ikiwemo Kiafya, Kiuchumi na Kijamii.

Mwandishi: Last Mlaki  toka NACOPHA