Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
TUME ya Taifa ya kudhibiti ukimwi (TACAIDS), inatarajia kuanza kampeni za kitaifa kuhamasisha wanaume kupima afya zao ,ili kujenga tabia ya kujitokeza kujua afya zao kwani ni asilimia 45 pekee ya kundi hilo walioaminika kuwa na VVU ndio waliopima kujua hali zao.
Aidha imeeleza ,kati ya watu kumi wenye maambukizi mapya kwa mwaka ,vijana wanne sawa na asilimia 40 ugundulika kupata maambukizi hayo.
Pamoja na hayo ,kati ya vijana kumi waliopata maambukizi mapya kila mwaka nane huwa vijana wa kike na wawili ni vijana wa kiume.IMG_9486
Mratibu wa mtandao wa viongozi wa dini wanaoishi na virusi vya ukimwi ,(TANERELA),mchungaji Amin Sandewa pichani .(picha na Mwamvua Mwinyi)
IMG_20180301_160202
Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti ukimwi (TACAIDS ) ,Leonard Maboko akizungumza jambo ,mjini Kibaha ,Mkoani Pwani ,katika mkutano ulioandaliwa na tume hiyo ,kupitia mipango ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli ya mwaka 2018/2019 .(picha na Mwamvua Mwinyi)
………………………………………………………………………

Mkurugenzi mtendaji wa TACAIDS ,Leonard Maboko aliyaeleza hayo mjini Kibaha ,Mkoani Pwani ,katika mkutano ulioandaliwa na tume hiyo ,kupitia mipango ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli ya mwaka 2018/2019 .
Alisema ,kampeni hiyo itakuwa ya miezi sita na itakuwa endelevu hadi hapo watakapohakikisha wanatokomeza ama kupunguza gonjwa hilo .
Maboko alisema  ,wale watakaobainika kuwa na maambukizi mapya watatakiwa kuanza tiba ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) mapema ili kuondoa vifo vinavyotokana na virusi hivyo .
Alielezea ,wanaandaa kampeni hizo kutokana na takwimu za utafiti wa viashiria vya ukimwi ya mwaka 2016/2017 inayoonyesha idadi ya watu wanaopima na wanaogundulika kuambukizwa wanaoanza kutumia dawa ni wanawake kuliko wanaume.
“Asilimia 45 ya wanaume ndio wanaoaminika kuwa wamepima na kujua hali zao ,hali ambayo inaonyesha ni kiwango cha chini “.
“Simaanishi wenye ukimwi wote wameshapima kujitambua ,lakini inahitajika hamasa ili tufikie malengo”alisema Maboko.
Hata hivyo Maboko alisema ,maambukizi mapya ya ukimwi yanaongezeka zaidi kwa kundi la vijana hususan wa kike .
“Hii inaonyesha huko kipindi cha nyuma hakukuwa na hali hiyo hivyo haina budi kundi hilo likatiliwa mkazo ,ili kupunguza ongezeko hilo ” 
“Hali ya maambukizi ya ukimwi Tanzania kwasasa ni asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.1 ,hali inapungua lakini inatakiwa tuendelee kupambana na maambukizi mapya ,na Tanzania bila ukimwi inawezekana” alisema Maboko.
Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo ,kuwa asasi mwamvuli zinarahisisha kazi ya uratibu kwa TACAIDS lakini changamoto waliyonayo ni kutopata ripoti za asasi hizo .
Nae mratibu wa mtandao wa viongozi wa dini wanaoishi na virusi vya ukimwi ,(TANERELA),mchungaji Amin Sandewa alisema wanawajengea uwezo wa kielimu viongozi wa dini wanaoishi na virusi hivyo ili kupambana na ukimwi na kuwa vielelezo kwa wengine.
Sandewa alisema, ugonjwa huo hauchagui ,muumini,viongozi wa dini wala mwalimu hivyo aliiomba jamii kuachana na unyanyapaa.
Meneja ufuatiliaji na takwimu ,kutoka baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (NACOPHA) ,Rachel Jacob alifafanua wanaratibu shughuli za masuala ya ukimwi kwa kulenga mtu mmoja mmoja,kundi na mtandao .
Kwa mujibu wake ,katika kufanikisha shughuli hizo wameshafikia halmashauri 154 nchini kwa kushirikiana na viongozi walioteuliwa ambao wana maambukizi kwa ajili ya kusaidia kuwafikia watu na vikundi hivyo .
Rachel alibainisha ,kwasasa wana wajumbe 616,984 miongoni mwao asilimia 44 ni wanaume waliojitokeza kuweka wazi afya zao .
Alifafanua zoezi hilo nao wanaendelea nalo ,kuhakikisha kufikia halmashauri zote hasa kundi la wanaume ambalo bado halina mwamko huo.
Katika mkutano huo ,asasi mwamvuli zilizoshiriki ni pamoja na NACOPHA,TAIFO,BAKWATA,
FAJISAM-PENTECOSTE,TANERELA,TEC,BAHAI,National Steering Committe, na TIENAI.