NA.MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji, Dorothy Mwaluko amewaasa Watanzania wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kuendelea kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo ili waweze kuishi maisha yenye afya na amani wakati wote.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI katika Konga ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoani alipowatembelea kukagua utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na namna konga hiyo inavyoendesha shughuli za uzalishaji Wilayani hapo Oktoba 17, 2019 Mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akizungumza na wajumbe wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wa KONGO ya Wilaya ya Kilombero alipowatembelea kuangalia namna wanavyoendesha shughuli zao za kimaendeleo na kuwajulia hali tarehe 17 Oktoba, 2019.

"Kipekee ninawapongeza kwa ujasiri wenu wa kujitokeza na kuonesha ulimwengu kuwa janga hili lipo na ni letu sote, kwani naamini hakuna mtu ambaye halijamgusa kwa namna moja au nyingine hivyo niwaombe mjitahidi kuendelea kutumia dawa hizi za kufubaza makali ya virusi ili kuendelea kuimarika zaidi,"alisema Mwaluko.

Baadhi ya wanachama wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU wa KONGA ya Kilombero awakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika ofisi za konga hiyo, Oktoba 17, 2019.
Aliwasisitiza kuendelea kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajatambua hali zao na wale waliotambua hali zao kuendelea kufubaza virusi na kutoacha kutumia  dawa hizo kwa kuzingatia umuhimu wake.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akizungumza na umoja wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wa KONGO ya Wilaya ya Kilombero alipowatembelea kuangalia namna tekeleza shughuli zao za kimaendeleo tarehe 17 Oktoba, 2019.

"Napenda kuwahamasisha msiache wala kuchoka kutumia dawa hizi kwa kuzingatia umuhimu wake katika kuhakikisha zinawapa nafuu na kuondoa magonjwa nyemelezi kuendelea kuwa na afya njema na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kufanya dunia mahali salama pa kuishi,"alisisitiza Mwaluko.

Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU wa Konga ya Kilombero, Halida Ally akisoma taarifa ya Konga hiyo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika konga hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela aklieleza kuwa, hali ya kiwango cha maambukizi Mapya ni asilimia 4.7 Kitaifa na maambukizi hayo ni mengi kwa wanawake kuliko wanaume hivyo Serikali itaendeelea kuhudumia kundi hili kwa kuhakikisha lilapewa dawa hizo kwa kadri itakiwavyo.

Mkurugenzi wa Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela akizungumza jambo kuhusu hali ya Maambukizi mapya kwa wanakonga ya Wilaya ya Kilombero wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko.


"Serikali imejipanga kuhakikisha kundi la WAVIU wote wanahudumiwa na kupatiwa mahitaji yao muhimu ikiwemo upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi (ARV) hivyo na kuhakikisha kundi kubwa la wanawake ambao ndiyo wanaoathiriwa zaidi linafikiwa kadiri iwezekanavyo na hii itaendeelea kusaidia kundi hilo kupunguza hatari ya kuingia katika maambukizi mapya,"alieleza Dkt.Kamwela.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akiangalia  baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na wanachanama wa KONGA ya WAVIU iliyopo Kilombero wakati wa ziara yake katika konga hiyo tarehe 17 Oktoba, 2019.
Aliongezea kuwa takwimu zinaonesha hali ya maambukizi mapya kwa kila mwaka ni watu 72000 ambapo kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 linaongoza kwa asilimia 40 na kueleza kundi la wanawake wanachangia asilimia 80 ya maambukizi hayo.
"Serikali imetoa kipaumbele kuwa mwitikio wa masuala ya UKIMWI umelenga kundi la vijana ili kupunguza maambukizi mapya yanayolikumba kundi hilo,"alifafanua Dkt.Kamwela.
Aliongezea kuwa wananchi wasipotambua hali zao mapema wanasababisha kuanza tiba kwa kuchelewa na hivyo kulazimika kuanza dawa wakati wa hatari na kuwalazimu kuwa na juhudi za ziada katika kutumia dawa ili kutokomeza maambukizi mapya na kufubaza virusi vya UKIMWI.

Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wa Konga hiyo Halida Ally alieleza kuwa hali ya utoro wa dawa imechangia kuongezeka kwa maambukizi mapya ambapo walifanikiwa kuhamasisha watu 30,712 kupima hali zao ambapo jumla ya watu 2,038 walikutwa na maambukizi kati yao wanawake ni 1,327  na wanaume ni 711.

Mwenyekiti wa Konga ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wilayani ya Kirombero Halida Ally akimuonesha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko bidhaa mbalimbali wanazotengeneza katika Konga yao ikiwa ni sehemu ya miradi inayowasaidia kujipatia kipato na kuinua uchumi wao alipotembelea konga hiyo Oktoba 17, 2019.
Alisema hali ya utoro wa dawa ni changamoto katika kuhudumia kundi hilo inayochangiwa na uwepo wa sababu mbalimbali ambapo katika kundi la WAVIU 2,038 wanaotumia dawa za kufubaza virusi ni 1,707 kati yao wanawake ni 1,034 na wanaume ni 673 katika kundi hilo watoro wa dawa ni 996 kati yao wanaume ni 335 na wanawake ni 673 hali ambayo inachangia kuongezeka kwa maambukizi mapya na kuongeza ukubwa wa janga hilo katika Halmashauri yao.

Naye mmoja ya wanachama wa konga hiyo Betina Januari aliipongeza Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ukimwi na kuahidi uendelea kutoa ushirikiano katika jitihada za kuwawekea mazingira wezeshi na kufikia malengo ya sufuri tatu ifikapo 2030.

KONGA Kilombero ni Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) ngazi ya Wilaya. KONGA ya Kilombero imeundwa mwaka 2013 ikiwa na vikundi 14 vyenye jumla ya wanachama 354 ambapo wanawake ni 237 na wanaume 117.

Mratibu UKIMWI mkoa wa Morogoro Bi. Ndayahunda Hendry akizungumza jambo wakati wa mkutano huo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)