Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha    na mapambano dhidi ya 

Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limeendesha warsha kwa WAVIU Washauri 75 kutoka halmashauri sita za wilaya mkoa wa Shinyanga ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).
WAVIU washauri ni watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na wamejiweka wazi na huru kuwashauri watu wanaoishi na VVU katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa,kutoa ushauri nasaha kwa wenzao,kujitolea kufuatilia na kufundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha sambamba na kuhamasisha WAVIU wenzao kujiunga katika vikundi ili kusaidiana na kupunguza unyanyapaa.
Warsha hiyo ya siku tatu imeanza Jumatatu Januari 29,2018 katika ukumbi wa Karena Hotel Mjini Shinyanga na kukutanisha pamoja WAVIU Washauri takribani 75 kutoka halmashauri za wilaya za Kishapu, Manispaa ya Shinyanga, Shinyanga, Kahama Mji, Ushetu na Msalala.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mratibu wa Masuala ya Watoto,Mama na Baba kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Aminael Tesha alisema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo WAVIU Washauri ili waweze kuwaunganisha wateja kutoka kwenye jamii kwenda kwenye vituo vya tiba na matunzo na kuwafuatilia wateja waliopotea katika huduma na kuwarudisha kwenye huduma.
“Kupitia warsha hii tutapeana mikakati mbalimbali jinsi ya kuwatafuta wateja waliopotea katika huduma na kujadili namna ya kuboresha zaidi huduma katika vituo vya tiba na matunzo lakini pia kutoa elimu kuhusu haki za WAVIU Washauri”,alieleza Tesha.
Naye Mratibu wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), kanda ya Mwanza, Veronica Joseph aliwasihi watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kujiweka wazi kwani itawasaidia kupata msaada kwa watu wanaowazunguka ikiwemo familia zao.
“Wale ambao hamjapima nawashauri mpime ili mjue afya zenu na ukibainika una maambukizi ya VVU jiweke wazi ili usaidiwe,kujiweka wazi kutakusaidia kuondoa matatizo na utaweza kupata fursa mbalimbali kutoka wafadhili”,alileleza.
Katika hatua nyingine alisema shirika la AGPAHI linatekeleza miradi ya Ukimwi katika mikoa sita nchini ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita,Mwanza, Tanga na Mara kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control and Preventation (CDC).

Mratibu wa Masuala ya Watoto,Mama na Baba kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Aminael Tesha akizungumza wakati wa warsha ya siku tatu ya WAVIU Washauri halmashauri sita za wilaya mkoa wa Shinyanga iliyofanyika katika ukumbi wa Karena Hotel Mjini Shinyanga.

Aminael Tesha akielezea malengo ya warsha hiyo.

Mwezeshaji katika warsha hiyo, Veronica Joseph ambaye ni Mratibu wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), kanda ya Ziwa, akielezea kuhusu umuhimu wa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kufubaza makali ya VVU na kujiweka wazi.

MVIU Mshauri, Joyce Philimon kutoka mkoani Simiyu ambaye anaishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 1997 akielezea umuhimu wa kujiweka wazi pale unapobaini kuwa umepata maambukizi ya VVU. Kujiweka wazi kwa Joyce kumfanya aishi salama na kwa amani na kupata fursa za kushiriki shughuli mbalimbali kutoka kwa wadau.  


MVIU Mshauri Seleman Habibu kutoka Kahama akielezea namna alivyoweza kuishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 2000 na ana watoto wawili ambao hawana maambukizi ya VVU na mke wake pia hana maambukizi ya VVU.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU katika Manispaa ya Shinyanga,Vedastus Mutangira akizungumza katika warsha hiyo ambapo akiwasisitiza watu wanaoishi na VVU kumeza dawa kwa utaratibu sahihi uliowekwa pamoja na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.

WAVIU Washauri wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yanajiri ukumbini.

Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini.

Mwezeshaji katika warsha hiyo,Vedastus Mutangira akitoa elimu kuhusu VVU na Ukimwi. Aliwasisitiza watu wanaoishi na VVU kumeza dawa kwa utaratibu sahihi uliowekwa pamoja na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.

MVIU Mshauri Neema Anthony kutoka kutoka CTC ya Segese katika halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.