Mwaka 2000 Tanzania ilitangaza UKIMWI kuwa
janga la Kitaifa. Katika kuimarisha juhudi hizi, mwaka 2004, serikali iliweka mpango wa upatikanaji bure
wa dawa za kufubaza makali ya VVU na kuhamasisha upimaji wa VVU. Hadi sasa kwa
mujibu wa takwimu zilizopo takribani watu 1,400,000 wanaishi na maambukizi ya
VVU na kati ya hao, takribani watu 850,000 wanatumia dawa (UNAIDS 2017). Yote
haya ni matokeo chanya ya juhudi za serikali ambazo zimechangia kupungua kwa
maambukizi ya VVU kutoka asilimia 8.3%
(2003) hadi aslimia 5.3% (THIMS 2012). Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi,
maambukizi ya VVU yanaonekana kuongezeka kwa kasi katika kundi la vijana wa
umri kati ya miaka 19 hadi 35 ukilinganisha na makundi mengine.
Katika hotuba yake Mheshimiwa. Rais
Dr. John Joseph Pombe Magufuli aliyoitoa
kwenye kilele cha maadhimisho wiki ya vijana,kumbukumbu ya kifo cha Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kuzima Mwenge wa Uhuru tarehe 14th October, 2017 huko
Zanzibar, kwa kunukuu maneno yake
mwenyewe alisema; “Vijana ndio uhai na
nguvu kazi ya taifa hili..; Taifa hili ni lenu..; Mjihadhari na tabia za matumizi
ya madawa ya kulevya na kufanya ngono zembe...” Kauli hii ya Mkuu wa Nchi
ni ya kupongezwa sana kwani inavunja ukimya ,kuamsha na kuhamashisha juhudi za
Kitaifa zinazolenga kufikia malengo ya 90-90-90
ifikapo 2020, vijana wakipewa kipaumbele.
Sisi Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) tumefarijika sana na kauli
hii ya Kiongozi wa Nchi kwa vijana. Tunaipongeza
sana.
Akimkaribisha Mheshimiwa Rais
kuongea na wananchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista
Mhagama alisema kuwa; mojawapo ya mafanikio ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka
2017 ni pamoja na kuhamashisha upimaji wa VVU kwa vijana. Katika mbio za Mwenge
za mwaka huu takribani watu 80,000 walijitokeza kupima na kujua hali zao
miongoni mwao wakiwemo vijana.
Kwa kupitia taarifa hii kwa vyombo
vya habari NACOPHA tunaomba pongezi zetu za dhati zimfikie Mhe. Rais Dr. John
Joseph Pombe Magufuli kwani ni imani
yetu NACOPHA kuwa kauli hii itaamsha upya ari na kuongeza kasi ya mwitikio kwa
UKIMWI kwa Viongozi na mamlaka zote za Serikali, mashirika ya kijamii , Wadau wa maendeleo , vyombo vya habari , viongozi
wa dini, jamii kwa ujumla na hasa vijana.
Ni ukweli usiopingika kuwa,
matumizi ya dawa za kulevya na ngono zembe ni vichocheo vikubwa vya maambukizi
mapya ya VVU na hasa kwa vijana. Vijana wengi na hasa wa kike wapo katika
hatari kubwa Zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kutokana na tabia hizi. Hata hivyo
kwa sasa ni vijana wachache sana wanaojitokeza kupima na kujua hali zao za afya. Hii ni changamoto kubwa
katika kufikia azma ya serikali kufikia malengo ya 90-90-90 ikiwa ni pamoja na
kujua hali yao ya maambukizi ya VVU; kuanza tiba; na kufubaza makali ya VVU. Ombi
letu Baraza kwa Mheshimiw Rais ni:
·
Kuendelea kuhamashisha juhudi za upimaji wa VVU ili kuhakikisha watu
wote wanaoishi na maambukizi ya VVU wanapima
na kujua hali zao za afya, wale wote wanaopatikana wanaishi na Maambukizi
wanaanza mara moja na kudumu kwenye tiba, na pia wote walio kwenye tiba wanafuasa
tiba kwa usahihi ili kufubaza makali ya VVU.
·
Kusisitiza na kusimamia viongozi wote kwa ngazi zote
kuendelea kuhimiza na kutoa adhari kwa wananchi wa makundi yote, kuepuka
maabukizi ya UKIMWI kwani bado Upo na maabukizi yanaendelea. Lengo ni kutokomeza
UKIMWI ifikapo 2030
·
Kutoa msukumo mpya na kuhuisha sera ya taifa ya
UKIMWI ya 2001 ili iweze kuendana na mikakati na uhitaji wa mwitikio wa UKIMWI
kwa sasa na hasa wakati huu wa awamu ya
Tano
·
Kuwawezesha WAVIU na hasa vijana kuwa na uhakika wa
kupata dawa kwa magonjwa nyemelezi kwani
kwa sasa dawa hizi hazipatikani na ni muhimu kwa ufuasi sahihi wa dawa
·
Kuhamasisha jamii kuondokana na Unyapapaa kwa WAVIU
kwani hiki ni kikwazo kikubwa kufikia malengo ya 90 90 90
Ni rai yetu kwa watanzania wote , kuwa
ni wajibu wetu sote , na hasa kwa kila kijana kuitikia wito wa mheshimiwa rais
kuhakikisha wanalinda afya zao kwa kuepuka na kujilinda na vishawishi na tabia
hatarishi kupata maambukizi ya VVU. Wazazi , walezi, Viongozi wa dini na wadau
wengine kwa nafasi zetu , kuumunga mkono Mheshimiwa rais na kuwa karibu na
vijana katika kuwaongoza na kuwaelimisha juu ya tabia hatarishi na kuwasaidia
kuepuka maambukizi ya UKIMWI na madhara mengine yatokanayo na Ngono zembe na
matumizi ya madawa ya kulevya.
Kwenu ninyi Vyombo vya habari, mnalo jukumu kubwa
kwa jamii, hususani vijana kuhakisha mnatoa taaarifa za mara kwa mara mkielimisha na kuhamsisha jamii kupata huduma
mbali mbali za kudhibiti UKIMWI na hasa
juu ya afya ya uzazi kwa Vijana. Napenda kusisitiza kuwa UKIMWI bado upo.
Tunapenda kutumia fursa hii
kuwashukuru wadau wote ikiwa ni pamoja na
Serikali yetu , Bunge la Jamuhuiri
ya Muungano wa Tanzania, USAID ,UNAIDS Mfuko wa Dunia wa UKIMWI, TB na Malaria,
Vyombo Vya habari na wengine wote kwa
kuliwezesha baraza kufanya kazi zake kwa ufanisi
Mwisho
kabisa, Tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais utayari wa Baraza na watu wanaoishi na VVU kwa ujumla
wetu katika juhudi za Serikali za kuimarisha afya za vijana ili washiriki
kikamilifu kuijenga Tanzania ya uchumi wa
Viwanda.
ASANTENI
SANA KWA KUNISIKILIZA.
Justine
Mwinuka
Mwenyekiti
Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na
VVU (NACOPHA)
Post a Comment