Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) kwa kushirikiana na  Ubalozi wa Marekani wazindua filamu ya Vijana kuhusu VVU na UKIMWI iitwayo ‘PILI” tarehe 8/11/2018 katika Ukumbi wa sinema Mlimani City, jijini Dar es salaam.


Filamu hii ni ya kwanza na yenye visa halisia vya kijamii inayoangazia maisha ya wanawake wanaoishi na VVU katika Afrika Mashariki. Ni mojawapo ya filamu chache zilizotengenezwa barani Afrika zinazohusisha wanawake ambao wengi wao si waigizaji.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huu alikuwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mohamed Bakari, ambapo pamoja na mambo mengine aliwahasa washiriki hasa vijana kuwa mstari wa mbele katika mwitikio wa UKIMWI.


Aidha wakati wa uzinduzi huo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk,Inmi Patterson amesema hii ni filamu ya Kitanzania iliyotambuliwa na matamasha makubwa ya filamu duniani inayohusu kuwatetea watu wanaoishi na VVU.

Akizungumzia filamu hiyo, Dk.Patterson amesema filamu hii imetengenezwa na vijana wa Kitanzania ikiwa imebeba maudhui ya kuwatetea watu wanaoishi na VVU Tanzania, ambapo waigizaji wake wengi ni wale ambao hawajapitia mafunzo rasmi.

Amesema filamu hii imeoneshwa  kwa mara ya kwanza Jijini London wiki chache zilizopita ambapo Matamasha makubwa ya filamu yameitambua filamu hiyo.

“Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 ya Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI nchini Tanzania, Ubalozi wa Marekani unashirikiana na Baraza la Taifa la Wanaoishi na VVU (NACOPHA) kwa ajili ya kuendelea kuionesha filamu hii katika Mikoa mbalimbali ambayo ni Mwanza,Mbeya,Njombe na Iringa,”amesema Dk.Patterson.

Pia Mkurungezi Mtendaji wa NACOPHA Ndugu Deogratius Rutatwa alihitimisha kwa kusema lengo kuu la uzinduzi wa filamu hii kwa Jiji la Dar Es Salaam na Mikoa iliyoteuliwa ni kukuza ongezeko na ufikiwaji wa huduma za VVU hususani kwenye tiba na matunzo miongoni mwa vijana wadogo wanaoishi na VVU kupitia kutambua mchango na msaada wa PEPFAR katika mwitikio wa Kitaifa wa UKIMWI kwa kutumia WAVIU kama wanufaikaji wa msaada kutoka PEPFAR nchini Tanzania.

Picha Mbalimbali za matukio yaliyokuwa yakiendelea wakati wa uzinduzi wa filamu ya PILI