Mkutano Mkuu wa tatu wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU ulianza mnamo tarehe 15 Novemba 2018 nakumalizika tarehe 16 Novemba 2018, katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Mkutano huo ulifunguliwa na katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,  Kazi, ajira, vijana, na watu wenye ulemavu Prof. Faustin Kamuzora aliyemuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa.

Serikali imewaahidi watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI nchini kutofumbia macho changamoto wanazokabiliana nazo na kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma za UKIMWI hapa nchini hayo yalisemwa kupitia hotuba  ya Waziri Mkuu wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa iliyosomwa kwa niaba yake na Prof. Faustin Kamuzora
Amesema kupitia hotuba ya mwenyekiti wa NACOPHA bwana justine Mwinuka alibaini changamoto mbalimbali zinazowakabili WAVIU ambazo ni pamoja na umbali wa vituo vya matibabu na kutumia muda mrefu kwenye vituo vya matibabu,kipato duni cha WAVIU kugharamia matibabu,lugha na vitendo vya unyanyapaa katika vituo vya kutolea huduma, uhaba wa mashine za kupimia wingi wa Virusi kwenye damu na kuratibu wadau wote kwa Ushirikishwaji wa WAVIU kwenye mwitikio wa UKIMWI kupitia muundo wa konga za WAVIU.

Aidha amesema katika kukabiliana na changamoto hizi, serikali imeendelea kufanya juhudi za kuzipunguza na hata kuzimaliza kabisa kwa kuongeza idadi ya vituo vya afya  vinavyotoa huduma ya matibabu ya VVU “hadi kufikia July 2018 tuna vituo visivyopungua 8000 vya kutolea huduma za matibabu ya VVU, pia tumeweza kusajiri WAVIU 839,544 kufikia mwishoni mwa mwaka 2017”
Mkutano huu umeenda sambamba na Baraza kutambua na kutunukia nishani za heshima kwa baadhi ya Viongozi kwa kutambua michango yao mikubwa katika mwitikio wa UKIMWI. 

Waliotunukiwa nishani hizo ni pamoja na Mhe, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa, Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, 

Mkurugenzi mstaafu wa TACAIDS Bi. Fatuma Mrisho, Mwenyekiti mstaafu wa NACOPHA bwana Vitalis Makayula na Mwenyekiti wa NYP+ Nevala Kyando.


Pamoja na hayo Mkutano Mkuu uliweza kuwachagua viongozi Bodi ya Baraza la Taifa la WAVIU ambapo wafuatao walichaguliwa kuwa viongozi wa bodi kwa nafasi ya Mwenyekiti ilitwaliwa na Bi Leticia Mourice Kapela wa konga ya Bukombe, Makamu Mwenyekiti bwana Yusufu Alfred Merere mweka hazina Mitterrand Mohamed Dagila  na wajumbe  Shamila Ibrahim, Elias Charles, Christina Martin, Deogratius Clevass, Francis Stolla, Hermes Mutagwaba, Pudensiana Mbwiliza na Amir Mahamud.




Mbali na uchaguzi wa bodi walichaguliwa pia wawakilishi wa WAVIU kwenye TNCM ambao ni Japhes Baitani na Pudensiana Mbwiliza

Mkutano mkuu wa NACOPHA hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kuwakutanisha wawakilishi kutoka Tanzania Bara na wadau wengine wa UKIMWI ukiwa na lengo la kutathimini utekelezaji wa Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kupata taarifa ya mwelekeo wa Baraza kwa kipindi kinachofuata na kujadiliana kuhusu mafanikio na changamoto zinazowapata WAVIU kote nchini  pamoja na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa  kufikia tisini tatu (90-90-90) .